Serikali
imehadharishwa juu ya uvamizi na wizi wa silaha katika vituo vya
polisi, kwa kuambiwa hali hiyo inatisha na kuhitaji hatua za makusudi
kuimarisha ulinzi nchini.
Aidha,
ilishauri polisi kwa kushirikiana na jamii iongeze jitihada na ibuni
mbinu mpya za kudhibiti wale wote wanaoendesha uhalifu na uuaji wa watu
wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe.
Baadhi
ya wabunge wameshauri Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), yaruhusiwe kusaidia Polisi kulinda raia
na mali zao, hususan kudhibiti vikundi vya kihalifu vinavyojitokeza.
Akichangia
taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama iliyowasilishwa
bungeni, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) alisema vituo vya polisi
kuvamiwa na majambazi na kuibiwa silaha, ni hali inayotisha
ikidhihirisha uhalifu ulivyokithiri nchini.
“Tuyaombe
majeshi mengine ya ulinzi ya nchi yasaidie jeshi la polisi. Kama
tuliweza kutumia majeshi mwaka jana kupambana na majangili, leo
tunashindwa nini kupambana na wahalifu hawa waliokithiri?
“Si
dhambi kutumia askari wa JWTZ au JKT kulinda nchi yetu. Eti wanajeshi
wetu wako nje ya nchi wanalinda wananchi, lakini ndani ya nchi yetu
wananchi wanaumia.”
Alisema
magenge ya kihalifu, wizi na uhalifu unaojitokeza unatisha sana. Alitoa
mfano wa kuibuka kwa kikundi cha Panya Road jijini Dar es Salaam na
kusema askari ama kwa uchache au kwa kukosa vitendea kazi, wanashindwa
kudhibiti uhalifu.
Alitoa
mifano mingine ya uhalifu ni pamoja kukithiri kwa wizi wa kutumia
pikipiki na kusema imefikia hatua, watu wanaoporwa wameviona vitendo vya
kawaida kwa kutokwenda kuripoti polisi.
“Kama
hatuwezi kuajiri askari wa kutosha kwenye jeshi la polisi tukawapa
vitendea kazi jeshi la polisi, wakapewa makazi bora, ulinzi au usalama
utakuwa katika hali ya hatari huko tuendako,” alisema.
Akihimiza majeshi kutumika kudhibiti makundi ya kihalifu yanayojitokeza kwenye jamii, mbunge huyo alisema, "Majeshi,
hasa JKT wako vijana wengi kambini. Kwa nini tusiwatumie? Tunaona shida
gani kuwatumia? Si suala la kukaa na kusema, kimataifa jeshi
hawaruhusiwi kulinda.”
Awali,
Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, katika taarifa ya utekelezaji wa
majukumu yake kati ya Februari mwaka jana na Januari mwaka huu, ilisema
ilibaini katika kipindi hicho hali ya ulinzi wa nchi na usalama wa raia
ilikuwa shwari.
Kamati kupitia kwa Mjumbe wake, John Chiligati ilipongeza jeshi la polisi kwa jitihada za kudhibiti uhalifu nchini.
“Kamati
ilipotembelea Mkoa wa Arusha iliridhika na hali ya kupungua matukio ya
uhalifu na pia ilikuta hali ya utulivu na amani imerejea katika Jiji la
Arusha,” alisema Chiligati.
Hata
hivyo, kamati ilishauri polisi itafute njia mbadala na za kisasa za
kupambana na kudhibiti uingizaji nchini wa dawa za kulevya, ukiwemo
usafirishaji bangi kwenda Kenya na uingizaji mirungi nchini kutoka
kutoka nchi hiyo.
ConversionConversion EmoticonEmoticon