.

Bundi awaandama Nyalandu, Lukuvi


  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
    Bundi wa majanga ameendelea kuwanyemelea mawaziri, safari hii wakitaka kichwa cha Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
    Nyalandu alituhumiwa kwa uzembe wa kushindwa kutoa tangazo kwenye gazeti la Serikali (GN), ambalo limesababisha Serikali kupoteza mapato ya zaidi ya Sh. bilioni 80.
    Aliyedai kichwa cha Nyalandu ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akitaka Waziri huyo amwandikie Rais barua ya kujiuzulu wadhifa wake, kwa kuikosesha serikali mapato hayo. Zitto alitoa hoja hiyo wakati akichangia mjadala uliohusu taarifa ya utekelezaji ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na ile ya Kilimo, Mifugo na Maji, zilizowasilishwa bungeni jana.
    Alisema kuwa tangu wiki iliyopta wabunge walikuwa wakilalamika kutopatikana kwa mapato ya Serikali kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini kumbe kuna mapato yanayopotea kutokana na uzembe wa Waziri huyo.
    Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2014, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, alisema Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), inapoteza Shilingi bilioni mbili kila mwezi kupitia tozo mpya kwa mfumo wa ‘fixed rate’ badala ya mfumo wa zamani ‘Concession rate’ katika kipindi cha kuanzia Septemba mwaka jana mpaka hivi sasa. Alisema Septemba 12, mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wamiliki wa hoteli zilizoko katika Hifadhi za Taifa dhidi ya Tanapa kupinga Shirika hilo kuanza kutoza tozo mpya kwa mfumo huo wa fixed rate badala ya mfumo wa zamani wa Concession rate.
    “Katika hukumu hiyo mahakama iliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa tangazo katika gazeti la serikali kuhusu kuanza kutumika kwa tozo mpya, ni takriban miezi minne sasa tangu kutolewa kwa hukumu hiyo, lakini tangazo hilo halijatolewa, hali ambayo inasababisha Tanapa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kupoteza mapato yanayofikia shilingi za Kitanzania bilioni mbili kila mwezi,” alisema Lembeli.
    Alisema kuwa tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo mwaka 2011 hadi Septemba 2014 Shirika la Hifadhi za Taifa limepoteza karibu shilingi bilioni 80 kutokana na kukosa malipo ya tozo hiyo.
    Lembeli alisema kuwa Kamati yake iliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii iwe imeshatoa tangazo hilo hadi kufikia Januari 28, mwaka huu, lakini mpaka hivi sasa tangazo hilo bado halijatolewa. Akichangia mjadala huo, Zitto alisema miongoni mwa mapendekezo ya Serikali yalikuwa ni mashirika mawili ya hifadhi ya Tanapa na Ngorongoro yawe sehemu ya wamiliki wa hisa za Shirika la Ndege la Tanzania ATCL ili kulikwamua shirika hilo la ndege kwa sababu utalii na ndege vinahusiana.
    Alisema Shirika la ndege ambalo kwa sasa lina hali mbaya kifedha, linahitaji fedha za kununulia ndege mpya, lakini bado taifa linapoteza mabilioni ya fedha kutokana na uzembe wa Waziri kwa sababu ya kutokusanya kodi ya kwenye tozo ya utalii.
    “Waziri Nyalandu yuko pale, anashindwa kutoa tangazo la Serikali, ili kodi hii iweze kukusanywa, tutaendelea mpaka lini sisi waheshimiwa wabunge kulalamika na kulalamika hatuchukui hatua…Mheshimiwa Spika naomba nitoe wito kwa Bunge lako tukufu, kufika jioni ya leo (jana), tutakapokuja kufanya majumuisho, kama tangazo la Serikali kwa ajili ya kukusanya tozo hizi halijatoka, Waziri awasilishe barua yake ya kujiuzulu kwa Rais,” alisema Zitto na kuongeza:
    “Hatutaki kuwa na mchezo na masuala ya fedha za umma, tunalalamika kila siku na kinachohitajika ni tangazo kwa ajili ya kukusanya all most two billions kila mwezi, tumeshapoteza eighty billions mpaka sasa… nakuomba tutakapofika jioni haujatoa tamko la tangazo hili, tusikuone humu bungeni kwa sababu hatuwezi kuvumilia upotefu wa mapato ya serikali.” 
    Kwa upande wake Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alimtaka Waziri Nyalandu kukabiliana na mamba pamoja na viboko ambao alidai kuwa wanaua na kuwatafuna watu ambao ndiyo wapiga kura wake jimboni badala ya kuendelea na harakati zake za kukimbilia Ikulu. 
    Alisema mamba na viboko hao wanashambulia watu na kuwaua kiasi cha kumaliza wapigakura wake huku akihoji kuwa ikiwa wapigakura wake watakwisha ni nani atamrejesha bungeni kwenye uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
    “Nilikwambia hapa bungeni kwamba wananchi wangu wa Mwibara wanateketea kwa sababu ya mamba, viboko, lakini mpaka leo haujafika kule, wapigakura wangu wanaendelea kutafunwa, nani atanirudisha bungeni kama wapigakura wangu wanaendelea kuliwa na mamba wako hawa,” alihoji Lugola.
    Alisema kuwa wananchi hao wakijaribu kupambana na viboko pamoja na mamba hao, wanakamatwa na askari kwamba wanaua wanyama ambao ni maliasili ya taifa, lakini serikali haiwasaidii kukabiliana nao ili wasiendelewe kuuawa.
    Lugola alimtaka Waziri Nyalandu kuitisha mkutano wa mamba na viboko waliopo katika eneo hilo na kuwazuia wasiendelee kuua watu ili kunusuru wapigakura wake jimboni.
    “Sasa nakuhakikishia, endapo hautafanya mkutano na hawa mamba na hutafanya mkutano na hao viboko, kuwaambia wasitafune wana-Mwibara, huko unakokimbilia, kama umeshindwa kutafuna mamba na viboko na sasa unakimbilia Ikulu, Ikulu kule ndiko utaweza?” alisema Lugola.
    NYALANDU AJIBU 
    Naye Waziri Nyalandu alisema baada ya hukumu, alitoa maagizo akielekeza kuwa tangazo hilo lichapwe kwenye gazeti la Serikali kabla ya Desemba mwaka jana.
    LUKUVI
    Lukuvi alidaiwa kumkingia kifua mwekezaji, ambaye amegoma kuilipa manispaa ya Kinondoni Sh. bilioni tatu kwa ajili ya kuendeleza viwanja vitatu vinavyomilikiwa na manispaa hiyo, jijini Dar es Salaam.
    Viwanja hivyo, vipo katika eneo la Oysterbay Villa, manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
    Lugola ambaye aliibua tuhuma hizo, alisema migogoro ya ardhi nchini imekuwa ni historia ya miaka mingi na kwamba, ni vigumu kwisha iwapo viongozi wa serikali watakuwa ndiyo wahusika wakuu wa kujihusisha nayo.
    Lugola alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakihodhi maeneo na wengine wakiwabeba kwenye mbeleko wawekezaji, ambao baadaye huzua migogoro baina yao na wananchi wa kawaida.
    Alitolea mfano wa mwekezaji huyo, ambaye alisema historia inaonyesha kuwa alifika katika eneo hilo na kuingia makubaliano ya kuviendeleza viwanja hivyo.
    "Na historia inaonyesha wakati mheshimiwa Lukuvi akiwa mkuu wa mkoa (wa Dar e Salaam) ndiye ambaye alihakikisha yule mwekezaji anapata lile eneo," alisema Lugola.
    Alisema wakati Waziri Lukuvi akiwa amefanya hivyo, ndiye huyo huyo tena amepelekwa kwenda kuongoza Wizara ya Ardhi ilihali mwekezaji huyo bado ana mgogoro na manispaa hiyo.
    "Mwekezaji yule ana kiburi, alizuia kamati ya Bunge isikanyage ardhi ya wananchi ya Watanzania ili tuweze kuona apartment 17, manisipaa ya Kinondoni," alisema Lugola.
    Aliongeza: "Mheshimiwa Spika, mheshimiwa Lukuvi, mwekezaji yule amehakikisha kwamba, Kinondoni hawatapata Sh. bilioni 3, ambazo anadaiwa. Na wewe ndiye unambeba kwenye mbeleko."
    "Pamoja na kwamba, mwekezaji huyo alizuia wabunge kuingia, alijifanya ni baunsa katika nchi hii, nikamwambia hapa amefika, nchi hii kuna mabaunsa ambao ni sisi. Nilihakikisha natumia ubaunsa wangu kuhakikisha kumdhibiti yule mwekezaji tukaingia kwenye vile viwanja viwili vya manispaa ya Kinondoni.
    "Nakuhakikishia mheshimiwa Lukuvi ukiendelea kumbeba kwenye mbeleko nitahakikisha naichoma moto na kuhakikisha huyu mwekezaji anadondoka."
    Alihoji sababu za serikali kutumia risasi, mabomu na virungu kuwapiga watu, kama kina Prof. Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi-CUF), akiwa ni mmoja wa waombelezaji waliokuwa wakiomboleza vifo vya wenzao badala ya kutumia silaha hizo kuwatandika wawekezaji fedhuli kama hao ili watoe fedha za Watanzania.
    LUKUVI AJIBU
    Akijibu hoja hizo jana jioni, Lukuvi alisema siyo yeye aliyesababisha mgogoro huo na kwamba alichofanya ni kuingilia kati na kuhakikisha majengo yanarejeshwa kwa Manispaa.
    Alisema alihakikisha pia mkataba wa miaka 99 wa awali unarekebishwa na kuwa wa miaka 47 na kusema kuwa mgogoro huo umekwisha na leo pande hizo mbili zitatiliana saini.

Previous
Next Post »