.

Escrow yataka vichwa vya Chenge, Tibaijuka, Ngeleja, Waitwa Tume ya Maadili kuhojiwa, Vigogo tisa kuhojiwa kwa kashfa hiyo


  •   Waitwa Tume ya Maadili kuhojiwa, Vigogo tisa kuhojiwa kwa kashfa hiyo
    Profesa Sospeter Muhongo.
    Baraza la Maadili limewaita kwa nia ya kuwahoji wabunge wanne, Profesa Anna Tibaijuka, Andrew Chenge, William Ngeleja na Victor Mwambalaswa kutokana na tuhuma za kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow.
    Wabunge hao ni miongoni mwa vigogo tisa wanaotuhumiwa kunufaika na fedha hizo  na watafika mbele ya Baraza hilo kuanzia Februari 23, mwaka huu.
    NIPASHE jana iliwatafuta wabunge hao bila mafanikio ili kujua kama wamekwisha kupokea wito wa kufika mbele ya Baraza.
    Mbali na watuhumiwa wa kashfa ya Escrow ambayo hadi sasa imesababisha kujiuzulu kwa mawaziri wawili, Profesa Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), pia Baraza hilo limewaita kwa ajili ya kuwahoji Meya wa Manispaa ya Tabora na Mkuu Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo. Huyu alihojiwa tena mwaka jana.
     Profesa Tibaijuka ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM) wakati Muhongo ni mbunge wa kuteuliwa.
    Baraza hilo litatoa uamuzi wa ama wahusika hao kufikishwe mahakamani au la, kulingana na hatia watakazokutwa nazo.
    Akizungumza na NIPASHE jana, Ofisa Habari wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Johanither Barongo, alisema mahojiano hayo yatafanyika kwa muda wa wiki tatu na yataongozwa na Jaji mstaafu, Hamisi Msumi na wajumbe wengine wawili, Hilda Gondwe na Celina Wambura.
    Barongo alisema Baraza hilo litafanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na litakuwa la wazi kumpa fursa mtu yeyote kushuhudia.
    Gambo na Meya wa Tabora watahojiwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
    Mbali na wabunge hao, Barongo alisema watuhumiwa wengine wa kashfa ya Escrow watakaohojiwa ni pamoja na majaji na wakurugenzi.
    Chenge ambaye ni mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), na Profesa Tibaijuka kila mmoja alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa James Rwegamalira wa VIP Engineering and Marketing Limited zikiwa ni mgawo wa Tegeta Escrow.
    Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema (CCM), alipata mgawo wa Sh. milioni 40.4. 
    Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini alilazimishwa kujiuzulu kutokana na kamati yake kushindwa kuisimamia Wizara ya Nishati na Madini juu ya kashfa hiyo.
    Viongozi wengine waliojipatia mgawo katika akaunti hiyo ni aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7), majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,  Profesa Eudes Ruhangisa (Sh. milioni 404.25), Jaji Aloysius  Mujulizi (Sh. milioni 40.4) na Mkurugenzi wa Wakala wa Usajili na Ufilisi (Rita), Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4).
    Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh. milioni 80.8). Kwa upande wake, Ofisa Sheria Mkuu wa Tume hiyo, Filotheus Manula, alisema wao wamewafikisha watuhumiwa hao katika Baraza hilo kulingana na sheria ya maadili ya viongozi wa umma inavyosema.
    “Kama sheria inavyosema, tunapopata malalamiko, tunapeleka mbele ya Baraza la Maadili ambalo huamua ni adhabu gani mtuhumiwa anaweza kuchukuliwa kulingana na sheria inavyosema na kulingana na namna atakavyokutwa na hatia,” alisema na kuongeza:
    “Ndivyo itakavyokuwa kwa hawa, kama watakutwa na hatia Baraza ndilo litaamua wapewe adhabu gani kulingana na sheria ya maadili ya viongozi wa umma inavyosema.”
    Manula alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1993, kifungu cha (8), kinasema kati ya adhabu ambazo viongozi wa umma wanaweza kuchukuliwa pale wanapobainika wamekiuka sheria za utumishi wa umma ni pamoja na kuonywa, kushushwa cheo na kusimamishwa kazi.
    Nyingine alisema ni kufukuzwa kazi na kushauriwa kujiuzulu; na kwamba hatua nyinginezo ambao Baraza linaweza kuwachukulia baada ya kuwakuta na hatia ni kuwafikisha mahakamani.
    Prof. Tibaijuka alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete Desemba mwaka jana wakati Chenge alijiuzulu Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
    Katika sakata hilo, wengine ambao hawahusiki katika shauri la Baraza hilo ambao walipata mgawo huo ni viongozi wa umma wastaafu ambao ni Daniel Yona ambaye alikuwa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, (Sh. milioni 40.4) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga, Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4).
    Kadhalika, wengine ambao siyo watumishi wa umma waliohusika katika mgawo huo ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam Eusebius Nzigilwa (Sh.milioni 40.4), Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh. milioni 80.8) pamoja na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh. milioni 40.4).
    Aidha, vigogo hao wanahojiwa wakati tayari kuna maofisa kadhaa wa Serikali ambao wamepandishwa kizimbani kwa kuhusika kwenye sakata hilo

Previous
Next Post »