.

Chopa ya Mwigulu yazua maneno

  • Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa hakijaruhusu kampeni, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ambaye amesema ameombwa na wazee na wasomi kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, sasa atazunguka nchi nzima kwa kutumia helikopta kufanya mikutano ya hadhara kuzungumza na wananchi.

    Hatua hiyo ya Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, ilitangazwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma jana.

    Msukuma alisema ameamua kumpa Mwigulu helikopta yake ili aitumie kuzunguka nchini kote kutokana na kuwa mtetezi wa wananchi na maslahi ya taifa kwa jumla.

    Alitangaza hatua hiyo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM Wilaya ya Morogoro mjini kwa ajili ya kuwashukuru wakazi wake kwa kuwachagua wagombea wa chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika hivi karibuni.

    Mgeni rasmi alikuwa Mwigulu aliyeambata na Msukuma kwa kutumia helikopta hiyo.

    “Tulianza ziara zetu Mkoa wa Tanga katika wilaya zote. Leo tumezunguka wilaya zote za Mkoa wa Morogoro na kumalizia hapa kwa chopa. Lakini tayari kumejitokeza majungu katika mitandao kuwa Mwigulu kanunua chopa ya kufanyia kampeni. Sasa nataka kuwaambia chopa ni mali yangu mimi Msukuma na ninampa Mwigulu atazunguka nayo Tanzania nzima kwa kuwa namuunga mkono kwa kutetea wanyonge na maslahi ya taifa hili,” alisema Msukuma.

    Aliongeza: “Kama kuna PCCB, polisi wanataka kumchunguza Mwigulu kapata wapi chopa ya kutembelea wasihangaike, waje kwangu mimi kuniuliza au waulize huko Geita Msukuma ni nani? Hii ni mali yangu halali na nimeamua mwenyewe kumpa kwa hiari yangu kutokana na kumuunga mkono kwa kuwa ni msema ukweli. Lakini siyo kumfanyia majungu Mwigulu katika mitandao ya kijamii tuliyoanza kuiona tayari.”

    Alisema Mwigulu ni mmoja wa viongozi wazalendo nchini kwa kutetea maslahi ya taifa na kupingana na viongozi wanaokandamiza wanyonge na matokeo yake kuifanya CCM ichukiwe na wananchi.

    Kuhusu vigogo waliohusishwa na kashfa ya uchotwaji zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Msukuma alisema wote waliohusika na kashfa hiyo wanapaswa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria bila kujali anatoka CCM.

    Alisema watu hao wanapswa kuchukulia hatua hizo kwa kuwa wao ndiyo chanzo cha Watanzania kuendelea kuishi katika hali ya umaskini na kusababisha kukichukia chama hicho.

    “Wote waliochota fedha za akaunti ya Escrow awe waziri au nani, tunataka wakamatwe na kushtakiwa ili kuwa mfano wa viongozi wengine. Wananchi hawawezi kuchukia chama chetu kwa sababu ya watu wachache waliokula fedha kwa manufaa yao,” alisema Msukuma.

    Kwa upande wake, Mwigulu alimshukuru Msukuma kwa kumpa helikopta hiyo ili kuzunguka nchini kuzungumza na wana CCM na Watanzania kwa jumla kuhusiana na mustakabali wa nchi pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali dhidi ya malalamiko ya wananchi.

    Kauli ya Msukuma kuhusiana na helkopta hiyo imefuatia mjadala katika mitandao mbalimbali huku baadhi ya watu wakidai kuwa Mwigulu ameinunua na wengine wakihoji hatua hiyo.

    Kuhusu sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, Mwigulu alisema wote waliochota fedha za umma hawatabaki salama.

    Mwigulu alisema wote watafikishwa mahakamani pamoja na wale waliokwepa kulipa kodi na kwamba, mchakato wa kukatwa kodi hiyo umekwishaanza.

    Alisema CCM haiwezi kumvumlia mtu yeyote aliyekula fedha za umma na na kuwataka wajiandae kuanzia sasa kwa kuwa hawatabaki salama, watafikishwa mikononi mwa vyombo vya sheria.

    Kuhusu wanafunzi wa programu maalumu stashahada ya ualimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kufikishwa mahakamani kutokana na kufanya maandamano bila kibali, alisema haikuwa busara kufanya hivyo kwa kuwa suala hilo lilipaswa kumalizwa ndani ya uongozi wa chuo, kwani walikuwa wakidai haki yao.

    Alisema katika kila vyuo kuna taratibu za kinidhamu, migomo na maandamano, hivyo badala ya kuwafikisha mahakamani wanafunzi hao, walipaswa kulimaliza tatizo hilo chuoni.

    Hata hivyo, Mwigulu aliwakikishia wanafunzi hao kuwa serikali imeshaanza kufanyia kazi madai yao na kwamba, kinachosubiriwa hivi sasa ni fedha, ambazo zikipatikana suala hilo litamalizika.

    Aliwataka wananchi wa Mkoa wa Morogoro kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wapigakura ili kupiga kura katika uchaguzi ujao kuchagua viongozi, ambao wana uchungu na nchi.

    Alisema suala la kujindikisha katika daftari hilo ni muhimu kwa kuwa litawafanya wananchi kuchagua viongozi watakaowataka na kuacha kulalamika baada ya uchaguzi kuisha.

    Kuhusu kukosekana dawa katika hospitali za mkoa wa Morogoro, alisema inashangaza kuona serikali imekuwa ikizinunua na kuzifikisha katika hospitali na vituo vya afya.

    Lakini akasema zimekuwa zikiibwa au kuuzwa katika maduka ya dawa ya watu binafsi, huku viongozi wa serikali wakiwapo pasipo kuwachukulia hatua wahusika na hivyo wananchi kulalamikia serikali.

    Alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi, kuhakikisha anasimamia tatizo la watumishi wasio waaminifu, ambao wanauza dawa za serikali kwa kuwachukulia hatua kali na kuwatataka pia wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwataja wahusika pale wanapowaona.

    Mwigulu akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini hivi karibuni, alisema amekuwa akipokea ujumbe mwingi kutoka kwa wazee wa Kijiji cha Butiama, mkoani Mara na kutoka kwa vijana wa vyuo vikuu, wakimuomba awanie urais mwaka huu, lakini suala hilo haliwekei umuhimu.

    Badala yake, alisema anatekeleza jukumu kubwa alilopewa na Rais Jakaya Kikwete la Naibu Waziri wa Fedha.

Previous
Next Post »