.

'Silaha za Boko Haram zatoka ndani ya jeshi la Nigeria'



Duru za kuaminika za ndani ya jeshi la Nigeria zimefichua kuwa, asilimia kubwa ya silaha za kundi la Boko Haram zinatoka ndani ya jeshi la nchi hiyo na wala hazitoki kwa mtandao wa al Qaida ambao unatuhumiwa kufanya vitendo vingi vya kigaidi katika nchi jirani za Chad, Niger, Mali na Mauritania. 

Televisheni ya lugha ya Kiingereza ya Aljazeera ya Qatar imezinukuu duru hizo za jeshi la Nigeria ambazo haikuzitaja jina zikisema kuwa, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba baadhi ya maafisa wa kijeshi wa nchi hiyo wanashirikiana na Boko Haram. 

Matamshi hayo yamekuja baada ya ripota wa televisheni hiyo kuripoti kutoka Nigeria kwamba, wanamgambo wa Boko Haram leo Jumapili wameanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno pamoja na mji wa Monguno wa jimbo hilo. 

Hadi tunaandaa habari hiyo, mapigano makali yalikuwa yanaendelea katika viunga vya Maiduguri kati ya jeshi na wanamgambo wa Boko Haram. Jeshi la Nigeria limekuwa likifanya pia mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo hao na kutekeleza pia sheria ya hali ya hatari katika mji huo. 

Kundi hilo la kitakfiri limeanza operesheni ya kuushambulia mji wa Maiduguri kutokea katika eneo la Njimtilo. Hivi karibuni pia kundi la Boko Haram liliripotiwa kufanya mauaji makubwa ya watu katika mji wa Baga, karibu na mpaka wa Chad baada ya kuuteka mji huo.

Previous
Next Post »