.

Wanafunzi wajawazito kuendelea na masomo wakijifungua


  • Serikali imeruhusu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopata ujauzito kuendelea na masomo wanapojifungua.
    Mratibu wa Masuala ya Jinsia wa  Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Ufundi, Chimpaye Marango, wakati wa mjadala wa sababu za kuongezeka kwa idadi ya watoto ya  mabinti wanaokosa elimu baada ya kupata mimba.

    Mjadala huo ulioitishwa na  asasi ya kiraia ya uchambuzi wa sera ya Policy Forum iliwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu.

    Marango alisema lazima wasichana waliopewa ujauzito kuhakikisha wanarudishwa haraka shuleni mara watakapojifungua, vinginevyo hatua kali watachukuliwa watakaowazuia.

     “ Wizara imeliona hilo na tayari imewekwa sera mpya, kwani kumuadhibu kwa kumfukuza shuleni hakutaweza kuwasaidia watoto wa kike kumudu maisha  badala yake tunaongeza umasikini ndani ya jamii,” alisema Marango.

     Awali, Dk.  Rebecca Balira, kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba Afrika (Amref) alisema tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike  limekuwa sugu nchini.

    Alisema katika utafiti uliofanyika katika Wilaya za Kilindi, Mkalama, Iringa vijijini na Same jumla ya wanafunzi wa kike 55,000  walishindwa kuendelea na masomo kwa kipindi cha mwaka 2003 hadi 2011.

    Dk. Balira alisema kwa upande wa shule za sekondari kwa muda wa miaka mitano inayoishia 2011 idadi ya wanafunzi waliopata mimba ilipungua kutoka asilimia 21 hadi 6.7.

    Kwa upande wa mwakilishi kutoka vyama vya kiraia, Mariam Asha , alisema kunahitajika juhudi ya kutoa elimu ya afya ya uzazi kuanzia ngazi ya shule ya msingi kutasaidia wanafunzi wajitambue na kukabiliana na vitendo hatarishi.

    Alisema kwa kupitia masomo hayo nguvu ielekezwe katika kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuwaelewesha wanafunzi wa kike hatari ya kupata ujauzito katika umri mdogo.

Previous
Next Post »