Rais Jakaya Kikwete.
Pia
wametilia mashaka utendaji wa Samuel Sitta aliyehamishiwa Uchukuzi
kutoka Ushirikiano wa Afrika Mashariki na William Lukuvi aliyehamishwa
kutoka Ofisi ya waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge kwenda Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakisema wizara hizo zina
changamoto nyingi kulinganisha na uwezo wao wa utendaji.
Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Christopher
Chiza, aliyehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji)
kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, nao wameelezwa kuwa
hawakupaswa kuacha katika baraza hilo kutokana na utendaji
usioridhisha. Yumo pia Anne Kilango aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango.
Aliyekuwa
Ofisa Mwandamizi wa masuala ya Biokemia wa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, Profesa Wakoti Nkya, ameyakosoa mabadiliko yaliyofanywa na
Rais Kikwete ya kumuondoa Dk.
Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi na kumhamishia Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki.
Alisema
kuwa hayana tija kwa taifa kwa kuwa yanalenga kumpunguza kasi baada
ya kutibua ‘madudu’ Mamlaka ya Bandari (TPA), Shirika la Ndege nchini
(ATCL) na Kampuni ya Reli (TRL).
“Mwakyembe
ameondolewa kwa sababu aligusa mizizi ya matajiri wachache baada ya
kuivuruga vuruga Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)ambayo imegeuzwa
shamba la bibi na akaanza kuwashughulikia vigogo hao kwa kuwasimamisha
kazi na wengine kuwafukuza…TRL nako alirejesha imani kwa wasafiri wa
treni baada ya kufanya maboresho makubwa, lakini ukweli kwamba alitoboa
mirija ya wajanja, ndiyo maana kapelekwa Afrika ya Mashariki,” alisema
Profesa Nkya.
Profesa
Nkya alisema kumuondoa Mwakyembe katika wizara hiyo kutarejesha nyuma
matumaini yaliyokuwa yameonekana ya kulifufua upya Shirika la Reli
nchini ambalo lilikuwa limetumbukia shimoni kutokana na changamoto
mbalimbali ikiwamo uduni wa miundo mbinu yake, kufa kwa mitambo na
kuziua njia za reli za kikaanda.
MHADHIRI IoU
Mhadhiri
Msaidizi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Iringa
(IoU), Emanuel Damalo, alisema kwa mabadiliko hayo, Watanzania
wasitegemee mashirika kama ATCL na viwanja vya ndege vilivyokuwa
vikisumbuliwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya huku kukiwa na juhudi
za makusudi za kuyaokoa yasiingie shimoni, zitaendelea kwa kuwa suala
la uzalendo ni la mtu binafsi.
Kwa
upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema
(Bavicha), Patrick Ole Sosopi, alisema mabadiliko hayo ya baraza la
mawaziri hayana tija, kwa kuwa baadhi ya Wizara zitalegalega kutoa
huduma kutokana na aina ya wanasiasa waliopewa kuziongoza kukosa utashi
na uzalendo wa kweli wa kutumikia umma.
MWENYEKITI ASAs
Mwenyekiti
wa Jumuiya za Wanataaluma Tanzania (ASAs), Paul Loisulie, alisema
mabadiliko hayo ni ya Rais na washauri wake ndio wanaojua sababu za
msingi za kuwaweka wahusika kwenye nafasi husika.
Hata hivyo, alisema baadhi ya watu akiwamo yeye amepokea kwa masikitiko uhamisho wa Dk. Mwakyembe kutoka Uchukuzi.
“Mnyonge
apewe haki yake, alijitahidi sana pamoja na ugumu wa maeneo kama
bandari, viwanja vya ndege (madawa ya kulevya), meli, reli, mabasi na
malori... Maeneo yote haya yanagusa maslahi ya watu binafsi, sina
uhakika wala matumaini kwamba anaeingia Uchukuzi atafanya vizuri zaidi
ya anayeondoka,” alisema Loisulie na kuongeza kuwa wakati ukifika
itajulikana.
Kuhusu Simbachawene kuchukua nafasi ya Prof. Muhongo, Mhadhiri huyo alisema anafaa kushika wizara hiyo kwa sasa.
Alisema
mamlaka ya uteuzi haijakosea kumpa nafasi hiyo. Hata hivyo, alisema
lazima awe tayari kufanya kazi na watu wote hasa wabunge bila kujali
itikadi za kisiasa na aepuke majigambo kama mtangulizi wake.
“Asikilize
maoni ya watu na kuyafanyia kazi, unyenyekevu utamsaidia sana katika
Wizara hii ngumu, Lukuvi (Willium) naye kwenye ardhi ana kibarua kigumu
sana lakini akijipanga anaweza akafanya vizuri,” alisema.
MWENYEKITI THTU-UDOM
Naye
Mwenyekiti wa chama wafanya kazi wa Elimu ya Juu tawi la Chuo Kikuu
cha Dodoma (THTU-UDOM), Nashon Maisori, alisema kwa jinsi Bunge
lilivyo Rais anapata wakati ngumu wa kupata mawaziri kutokana na baraza
lake kubadilishwamara kwa mara kufuatia mapungufu ya mawaziri.
“Mweshimiwa
Rais amejikuta hana watu tena wa kuwapa uwaziri, inabidi tu sasa
awekwe mtu kujaza nafasi na siyo lazima awe ana uwezo... Ila suala la
Mwakyembe, mimi binafsi nimeshtuka sana, sikutarajia aondolewe Wizara
ya Uchukuzi kwa sababu kwa mtizamo wangu alikuwa anafanya kazi nzuri
sana,” alisema.
Aliongeza:
“Hata kwenye mpira kocha humpumzisha mchezaji aliyechoka na siyo
mchezaji anayetegemewa uwanjani. Kumpeleka huko Afrika Mashariki ni
kupoteza mchapa kazi mzuri na kumpa kazi laini, mawaziri ambao walikuwa
wakichapa kazi sana ni Magufuli na Mwakyembe tu wengine business as
usual.”
CHAUMMA
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma),
Kayumbo Kabutari, alisema Baraza hilo ni la kivivu la bora wamalize
salama inavyoelekea Kikwete amebanwa ndani ya chama chake na makundi ya
urais yanayomhofia Mwakyembe ambaye ametengeneza jina kupitia Wizara ya
Uchukuzi.
“Hivyo
wamfiche Simbachawene ni mwendelezo wa kuficha uozo wa wizara husika
hakuna asilolijua la kifisadi kwani alikuwa msaidizi wa karibu wa
Muhongo upande wa nishati naibu waziri waliingia pamoja na Muhongo,”
alisema Kabutari.
Kuhusu
Lukuvi, alisema ameshindwa kutatua mgogoro mdogo wa ardhi wa Mamlaka
ya Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) katika Manispaa ya
Dodoma na wananchi, hivyo hataweza kushughulikia migogoro mikubwa ya
ardhi nchi mzima,” alisema.
“Hakuwatendea
haki Watanzania kwa kumuondoa Dk. Mwakyembe Wizara ya Uchukuzi ambayo
alikuwa anakwenda nayo vizuri na kumuingiza Sitta ambaye alikuwa Afrika
Mashariki,” alisema Wachacha Peter, mkazi wa Mabatini, jijini Mwanza
na kuongeza kuwa Rais Kikwete amerudisha nyuma maendeleo ya uchukuzi
baada ya kumuondoa Dk. Mwakyembe na kumuingiza Sitta aliyekuwa Wizara
ya Afrika Mashariki.
Alisema
Wizara ya Uchukuzi ambayo inahitaji waziri mwenye kasi, inaweza
kurudisha nyuma juhudi za wizara hiyo ambazo zilianza kuonyeshwa na
Waziri Mwakyembe katika kufufua reli ya kati.
Hata
hivyo, mkazi huyo alisema wizara nyingine zimefaanikiwa kupata
watendaji wazuri ingawa wapo mawaziri ‘mizigo’ walioachwa na kupelekwa
wizara nyingine.
Naye
mdau wa siasa wa jijini Mwanza na mkazi wa Nyakato, Peter James,
alisema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kikwete hayana tija kwa
Watanzania kutokana na baadhi ya wizara kiupelekewa mawaziri ‘mizigo’.
“Hakuna
jipya alilofanya Kikwete zaidi ya kuzidi kuzipa wizara nyingine mizigo
kutokana na kupelekewa watu ‘mizigo’...lakini kwa kipindi kilichobaki
cha miezi sita hawatafanya lolote la maana,” alisema James.
Alisema
kufanya uteuzi wa haraka haraka bila kuwafanya tathmini ya utendaji
wao, Rais Kikwete anazidi kuwaongezea kero wananchi kwa kuwapo na
mawaziri wasiowawajibikaji.
Hata
hivyo, mkazi wa Buhongwa nje kidogo na Jiji la Mwanza, Christopher
Chacha, alisema hashangazwi na mabadiliko hayo ya Kikwete kutokana na
kushindwa kuwaondoa mawaziri kama Dk. Shukuru Kawambwa na Christopher
Chiza.
JUKATA
Kaimu
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda,
alisema babadiliko hayo yamefanyika kikiwa kimebaki kipindi kifupi cha
serikali ya awamu ya nne kuondoka madarakani, hivyo Watanzania
wasitarajie mambo mapya.
“Hapo yamefanyika mabadiliko ya sura, hakuna jipya, kipindi kimebakia kifupi sana Watanzania wasitarajie jipya,” aliongeza.
DK. BANA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema zipo
Wizara ambazo zinahitaji utendaji wa hali ya juu na uzoefu katika
kazi, hususani Wizara ya Uchukuzi na Nishati ambazo alisema kwa uteuzi
ulifanyika haamini kama kutakuwa na mabadiliko yoyote.
Alisema
ameshangazwa na mabadiliko katika Wizara ya Uchukuzi kwa kuhamishwa
Dk. Mwakyembe ambaye alionyesha mwanga kidogo wa kushughulikia
changamoto zinazoikabili wizara hiyo nyeti.
“Nimeshaganzwa
na uteuzi wa Dk. Mwakyembe kupelekwa Wizara ya Afrika Mashariki,
wakati kuna matatizo makubwa ndani ya Wizara ya Uchukuzi ambayo alikuwa
ameanza kuyashughulikia ambayo alipaswa aendelee ili ayamalize,
ikiwamo suala la ATC, Bandari na kashfa zilizokuwa zinaendelea Uwanja
wa Ndege,” alisema Dk. Bana na kuongeza:
“Ninavyoamini
Wizara ya Afrika Mashariki anakwenda kupumzika tu kwa sababu haina
kazi nyingi kama ilivyo ya Uchukuzi, ninashindwa kuelewa ni kwa nini
ametolewa pale anajua Rais mwenyewe, lakini mimi naona Dk. Mwakyembe
alifaa sana Uchukuzi.”
Aliongeza
kuwa Sitta ni mtendaji mzuri, lakini kwa sababu Dk. Mwakyembe alikuwa
ameanza kufanya kazi nzuri, ni vema angeendelea nayo ili kuhakikisha
inakaa sawa.
Akizungumzia
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzi ya Ufundi, Anna Kilango, alisema
haamini kama ataweza kuimudu wizara hiyo kwa kuwa uwezo wake ni mdogo.
Alisema
hana imani kama Kilango ataweza kumshauri vizuri waziri wake kwa kuwa
ni mwanaharakati na kwamba uharakati na kazi aliyopewa haviwezi
kwenda pamoja.
Kuhusiana
na Wiazara ya Nishati na Madini, ambayo amepewa Simbachawene, alisema
Wizara hiyo ni muhimu na ambayo inahitaji mtu mzoefu na mchapakazi,
lakini anaamini endapo atafanya kazi kwa bidii ataiweza.
DK. SLAA
Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod
Slaa, alisema watanzania wasitarajie matumaini yoyote katika uteuzi
huo.
Akimzungumzia
Lukuvi, alisema wakati akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge) alikuwa chanzo cha kukwamisha mchakato wa Katiba, hivyo
kumpeleka katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi ni kusababisha
matatizo.
“Kwa
ujumla hata kwa hatua ambayo Tanzania imefikia kwa sasa huwezi
kutegemea kwamba yupo kiongozi yeyote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ambaye atawaletea matumaini Watanzania, wote, ni matatizo matupu hakuna
mwenye nafuu, eti unamtoa Waziri ambaye hata chama chake kinamwita
mzigo unamhamishia Wizara nyingine,” alisema Dk. Slaa bila kuwataja.
Hata
hivyo, tangu mwaka juzi Katibu Mkuu wa CCM, Abdurlahman Kinana na
Katibu Mwenezi, Nape Nnauye katika ziara zao za kuhimiza utekelezaji wa
Ilani, wamekuwa wakiwataja kwa majina baadhi ya mawaziri kuwa ni
mizigo. Miongoni mwao ni Chiza na Kawambwa.
Dk.
Slaa alimtolea mfano Anna Kilango kwamba anadaiwa kuwa na kashfa ya
kuuza kiwanda cha Tangawizi katika Jimbo la Same Mashariki, lakini
anashangaa kuteuliwa kuongoza wizara muhimu.
PROF. BAREGU
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Profesa Mwesiga Baregu,
alisema uteuzi wa Rais umeonyesha wazi kuwa amekosa timu ya mawaziri
wa kufanya nao kazi.
Alisema ni mara ya tano Rais anabadilisha Baraza la Mawaziri na kila anapofanya hivyo hakuna mabadiliko yeyote yanayoonekana.
“Mabadiliko
haya ya Baraza la Mawaziri, yanaonyesha kuwa Rais amekosa timu ya
Mawaziri wa kufanya nao kazi, hana uwanja mpana wa kumsaidia kupata
watendaji, hii ni kwa sababu ya Katiba ambayo inamruhusu kuteua ndani
ya Bunge tu wakati watendaji wengine wazuri wako nje ya Bunge,”
alisema Profesa Baregu.
Aliongeza:
“Na ndiyo maana wananchi walipendekeza kwa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kwamba Mawaziri wasiwe Wabunge, hii ingempa Rais
wigo mpana na angepata watendaji wazuri, tofauti na ilivyo sasa, Rais
anakosa watendaji kwa hiyo anakuwa anazunguka mle mle, anamteua Waziri
anashindwa hapa, anamjaribu pengine kwa sababu tu anakosa watu, na
jambo hili ni hatari. Kwa hiyo hata mimi siwezi kusema nani ataweza na
nani atashindwa kwa sababu wengine tulisema wanaweza, lakini
wameshindwa.”
DK. SEMBOJA
Mhadhiri
wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Haji Semboja,
aalisema ana imani na Sitta kutokana na uadilifu na utendaji wake kazi
serikalini na kuwa lisema ili Sitta afanye kazi kwa usahihi, anahitaji
ushirikiano kati yake na watendaji wa wizara nzima.
“Mawaziri
wengi wanashindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa sababu ya
kutopewa ushirikiano na watendaji, hali inayopelekea kuenguliwa nafasi
zao,” alisema Dk. Semboja.
Kuhusu
Simbachawene, alisema kinachotakiwa kufanyika ndani ya wizara hiyo ni
kumpa ushirikiano ili aweze kutatua changamoto zilizomo na kufufua
matumaini ya Watanzania.
Aidha, alisema hana wasiwasi na utendaji kazi wa Wasira kwa kuwa anafahamika kwa umakini wake kazini.
Aliongeza kuwa, bado ana wasiwasi na uteuzi wa Lukuvi kwa kuwa mara nyingi amekuwa akituhumiwa kwa utendaji usioridhisha.
“Natilia
shaka utendaji wa kazi wa Lukuvi, ni bora Rais angemteua Naibu Waziri
wake (Angela Kairuki) kuchukua nafasi, hapo nisingetilia shaka uteuzi
uliofanyika,” alisema.
NYAKEKE WA TRAWU
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), alisema
haungi mkono mabadiliko hayo hususan wale waliohamishwa kwenye wizara
zao akiwamo Dk. Mwakyembe na Sitta aliyepelekwa kuchukua nafasi yake.
Alisema
kubadilishwa kwa mawaziri wenye utendaji mzuri kama Dk. Mwakyembe
kunarudisha nyuma utendaji na maendeleo ya wizara husika ambayo
yalikuwa yameanza kuonekana na kwamba kwa kuwa uchaguzi mkuu
umekaribia, ingekuwa vizuri kuwaacha katika wizara zao.
Kubadilishwa
kwa Baraza hilo la Mawaziri kumetoka na Waziri aliyekuwa anaiongoza
Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kujiuzulu na
aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka, kufutwa kazi kutokana na kashfa ya akaunti ya
Tegeta Escrow. Imeandikwa na Godfrey Mushi, Moshi; Augusta
Njoji,Dodoma; Daniel Mkate, Mwanza; Christina Mwakangale, Elizabeth
Zaya na Hussein Ndubikole, Dar.
CHANZO: NIPASHE
ConversionConversion EmoticonEmoticon