.

Majambazi wapora tena bunduki, risasi za Polisi


  • Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki
    Matukio ya uporaji silaha yameendelea kuliandama Jeshi la Polisi  nchini baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kuwapora askari wake bunduki mbili aina ya SMG kisha kumjeruhi kwa kumchona kisu mmoja wao.
    Tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana katika Jiji la Tanga,  pia lilihusisha uporaji wa risasi kutoka kwa walinzi hao wa usalama wa raia na mali zao.
    Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, akizungumza na NIPASHE, alisema kuwa  tukio hilo lilitokea juzi saa 5:15 usiku katika eneo la barabara ya tano mjini Tanga.
    Kamanda Ndaki alisema katika tukio hilo, askari mmoja PC Masoul alichomwa kisu na amelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bomba kwa matibabu.
    Alisema askari huyo alipata mkasa huo wakati akiwa na mwenzake PC Mwalimu wakiwa katika doria mjini Tanga na ghafla walivamiwa na watu 
    ambao wanasadikiwa kuwa majambazi kisha kuwapora bunduki hizo.
    “Tumeanza upelelezi wa tukio hilo na hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pia imekaa kujadili tukio hlo,” alisema Ndaki.
    Taarifa zaidi kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kuwa askari hao waliporwa silaha hizo walipokwenda kula chips katika eneo hilo na baada ya kumaliza walipoanza kuondoka ndipo walipovamiwa na majambazi .
    Chanzo chetu cha habari kinaeleza kwamba kabla ya kuporwa bunduki hizo askari hao walipigwa ili kuwashinikiza  kukubali kuziachia.
    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fresser Kashai, alipotafutwa kutoa maelezo zaidi kuhusiana na tukio hilo, alisema yuko nje ya mkoa. Kashai anahudhuria mkutano wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi mjini Dodoma uliofunguliwa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
    Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku saba tu tangu majambazi walipokivamia  kituo cha polisi Ikwiriri wilayani Rufiji, mkoani Pwani na kuwaua askari wawili na kuiba bunduki saba.
    Katika tukio hilo, majambazi hao ambao walidaiwa kuwa zaidi ya 10 waliiba bunduki aina ya SMG mbili, SAR mbili, Shortgun moja na bunduki mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
    Askari waliouawa ni PC Judith Timoth na Koplo Edga Mlinga, hadi sasa Jeshi la Polisi halijatoa maelezo kuhusiana na msako unaoendelea kama kuna watuhumiwa waliokamatwa, licha ya Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), Ernest Mangu, kutangaza bingo ya Sh. milioni 20 kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazowezesha kuwatia mbaroni waliohusika. 
    CHANZO: NIPASHE

Previous
Next Post »