Dar es Salaam.
Miezi michache baada ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa
nchi, watumishi wawili waandamizi wa Serikali wamefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakituhumiwa kupokea
rushwa ya mamilioni ya fedha zilizotoka kwenye akaunti hiyo.
Mahakama
hiyo ilielezwa jana kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliwekewa
kiasi cha Sh323 milioni kupitia akaunti yake namba 00120102602001.
Kadhalika,
Mahakama ilielezwa kuwa Februari 12, 2014, Mhandisi Mkuu wa Wakala wa
Umeme Vijijini (Rea), Wizara ya Nishati na Madini, Theophillo Bwakea
alipokea rushwa ya Sh161,700,000 kupitia akaunti yake namba
004101102643901.
“Upelelezi
wa kesi umekamilika naomba mahakama izuie akaunti ya mshtakiwa
iliyotumika kupokea fedha hizo za escrow na kesi ipangwe kwa ajili ya
kusomewa maelezo ya awali,” alisema Leonard Swai ambaye ni Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma
hati ya mashtaka katika kesi namba 11 ya mwaka 2015 inayomkabili
Mujunangoma, Swai alidai mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo kinyume na
kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kupambana na Rushwa, Namba 11 ya mwaka
2007.
Swai
alidai kuwa Februari 5, 2014 katika Benki ya Mkombozi iliyopo wilayani
Ilala, Dar es Salaam, Mujunangoma akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria
wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipokea kiasi hicho
cha fedha kutoka kwa James Burchard Rugemalira, ambaye ni mshauri huru
wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya
Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa
muda wa kampuni hiyo.
Baada
ya kusomewa shtaka hilo, Mujunangoma alikana na mwendesha mashtaka
huyo wa Takukuru alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha sheria
anachoshtakiwa nacho, mshtakiwa huyo hahitaji kibali kutoka kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu
Emilius Mchauru alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili
wanaofanya kazi katika taasisi ya Serikali na kwamba kila mdhamini
asaini hati ya maneno ya Sh10 milioni.
Pia,
Hakimu Mchauru alimtaka mdhamini ama mshtakiwa mwenyewe, kuwasilisha
mahakamani hapo nusu ya fedha taslimu anazodaiwa kuzichukua kama
rushwa, ama kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya
kiasi hicho cha fedha.
Hata
hivyo, baada ya kutolewa kwa masharti hayo, mshtakiwa alipata
wadhamini wawili wanaoaminika , kutoa hati mbili za mali isiyohamishika
ambazo alidai zina zaidi ya thamani ya fedha iliyomo ndani ya hati ya
mashtaka.
Kuhusu
kuzuia akaunti ya mshtakiwa, Hakimu Mchauru aliutaka upande wa
mashtaka kuwasilisha maombi mahakamani hapo na kuyaambatanisha na hati
ya kiapo itakayounga mkono maombi hayo.
Kwa
upande wa Bwakea, aliyefunguliwa kesi namba 12 ya 2015, Swai alidai
kuwa siku hiyo ya tukio katika benki ya Mkombozi alipokea rushwa ya
kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake.
- Mwananchi
- Mwananchi
ConversionConversion EmoticonEmoticon