.

ALiomba fedha aliponyimwa, akamtukana mwenye duka...


  • Sema magharibi ya London siyo sawa na ya Afrika Mashariki. Majira yanapobadilika na mwangaza wa jua kutumbukia;  huja na mbwembwe zake. Tuko msimu wa baridi kali yenye barafu  ukanda wa kaskazini wa dunia. Kiza huanza kukonyeza saa tisa alasiri. Hiyo saa kumi na moja jioni tunayosimuliana giza finyu lilishapiga deki. Mchana, kwaheri. Lakini shughuli za wanadamu zilezile. Maduka hayajafungwa. Duka tunalotazama ni la hawa wamachinga pembe ya barabara kuu. Wahindi wenye maduka wanajuana kwa vilemba. Mmachinga wetu ni  Mpakistani. Ana kameza kake kadogo mbele ya upenu wa mita tano kwa mapana ya mita moja, kajaza simu za mkononi, vibiriti, sigara.  Jambo la ziada ni simu na vipengele vyake. Betri, waya, mikebe ya kuzifungia; kila unachokililia kwa simu yako;  ongeza yeye fundi.
    Iko siku aliniambia kwao alihitimu ualimu ila sababu ya rabsha za kisiasa akatupilia mbali taaluma yake akafuata ndugu aliowajua  London. Ukimchunguza hajafikisha miaka ishirini na tano. Yuko hapa miaka miwili. Alianza kaduka bila meza na mifuko ya plastiki. Akiuza kadi za Lyca Mobile, kampuni ya bei rahisi inayotumiwa sana na wageni  Uzunguni. Mtanzania anapopiga simu kutoka huku mara nyingi anatumia mtandao wa Lyca.  Simu za viganjani ni biashara nzuri. Tuseme suala zima la kompyuta na mitandao ni kitengo chenye masilahi.
    Watazameni vijana wawili waliounda WhatsApp. Mmoja kwao ni Ukraine. Walianza kitu kidogo tu lakini leo mabilionea  baada ya kumuuzia Myahudi anayemiliki Facebook uvumbuzi wao.  Vijana wa Kitanzania mnaosoma kuweni wabunifu. Jaribuni kutafiti na kujua nini kinatakiwa. Uchunguzi wa kina badala ya  domo sana na siasa za malalamiko.
    Basi, Mpakistani alichangamkia umachinga na hizo kadi.  Baada ya miaka miwili, hauzi tu vidato vya simu. Anazikarabati. Ukimuuliza kajuaje, atakwambia alipofika  Uingereza alikwenda chuo akasomea ufundi  miezi kumi. “Mengine ni utundu tu...” Kaduka hakiishi wateja. Hula hapo hapo,  kutwa, kasimama akichora  fedha.
    Siku hii tunayohadithiana nilitaka asafishe mfereji wa simu yangu uliokuwa na mushkeli. Wakati nimetoa pochi  n’namlipa paundi tano alizotaka (kama shilingi elfu kumi na mbili); kando yangu kajipachika bonge la mtu. Mwamba. Niliisikia sauti yake nzito kabla ya kushuhudia tambo lake. Macho yanakodolea zile fedha ninazomlipa Mpakistani.
    “Nipe paundi moja nikanunue maji. Nitakurudishia.”
    Kamngurumia Mmachinga. Sauti nzito.  Ilinikumbusha mchezaji fulani wa sinema. Nilipogeuka nikamaizi nimemfikia begani. Mweusi sana. Hajavaa nguo chafu. Yuko kawaida. Kiingereza chake kina lafudhi hakika ya Kiafrika.  Mpakistani kamwambia hana hiyo paundi moja ambayo ni kama ya shilingi elfu mbili na kitu za Tanzania.
    “Nipe bwana nitakurudishia!” Jamaa kazoza, na kusonya juu.
    Hapo sasa ananizonga na miye maana kanafasi tulichosimama wawili hakitutoshi. Kawaida huku Uzunguni mteja anapokuwa akihudumiwa, wale wanaomfuata  husubiri zamu yao katika foleni. Hivyo jamaa hajafuata utaratibu. Ongeza kiburi.
    Mpakistani kapokea fedha niliyompa. Akaiweka kibindoni. Upesi akachakura  makabrasha nyuma ya bidhaa zake, akarejea na chupa ndogo ya maji. Akampa jamaa. Bure.
    “Haya chukua, maji. Hela sina, samahani.”
    Ombaomba si kapewa maji aliyotaka? Sasa...
    - Mwananchi

Previous
Next Post »